Abstract:
Kila lugha ina mchango wake katika maendeleo na wingilugha unaweza kuathiri maendeleo kwa njia chanya au hasi. Utafiti huu uliongozwa na madhumuni matatu: kuchanganua ruwaza za matumizi ya lugha katika Kaunti ya Machakos, kutathmini uhusiano na athari za lugha mbalimbali katika utekelezaji za maendeleo na kutambua nafasi ya mielekeo katika uteuzi wa lugha mahsusi za kuundia na kuwasilishia sera za maendeleo katika Kaunti ya Machakos. Msingi wa kifalsafa wa utafiti huu ulijengwa na nadharia mbili; Kiunzi cha Kinadharia cha Lugha na Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi na Nadharia ya Utendaji Razini. Ili kufikia lengo hili, utafiti huu ulitumia muundo mseto huku muundo afikivu mseto ukitumika kufasili data za kitaamuli na zile za kitakwimu.Sampuli ya utafiti huu ilihusisha watafitiwa 146; wananchi 142 kutoka kwa vijiji sita vilivyotabakishwa na waundaji sera wanne kutoka kwa idara nne lengwa. Kwa msingi kuwa huu ni utafiti mseto, uchunguzi huu ulitumia mbinu nasibu na zisizonasibu za usampulishaji. Usampulishaji utabakishaji sinasibu ulitumika kuteua vijiji lengwa sita huku usampulishaji nasibu sahili ukitumika kuteua kadiri ya asilimia ya sampuli ya kila kijiji. Mbinu ya usampulishaji kimakusudi ilitumika kuteua viongozi wa idara nne lengwa. Utafiti huu ulitumia vifaa vya hojaji funge na nusu-funge, dodoso nusu-funge, mwongozo wa uchunzaji na kiunzi cha kuchanganulia nyaraka zilitumika kukusanya data. Zanatepe ya
Kichanganuzi Data za Kitakwimu za Sayansi Jamii ilitumika kuchanganua data za kitakwimu huku uchanganuzi kidhamira ukitumika kuchanganua data za kitaamuli. Ili kuhakikisha uthabiti na uhalali wa utafiti na vifaa vya ukusanyaji data, utafiti wa majaribio ulifanywa katika eneo la Kitengela na uhalali wa maudhui kufanywa kwa vifaa husika mtawalia. Matokeo yalionyesha kuwa katika maeneo vizingasifa ya mashinani, lugha ya Kikamba na mseto wa Kikamba na Kiswahili ni maarufu zaidi huku lugha za Kiingereza na Kiswahili zikiwa maarufu zaidi katika maeneo vizingasifa ya mjini na kuwa zina athari
chanya kwa utekelezaji wa maendeleo katika maeneo husika. Mielekeo chanya kwa lugha ya Kikamba katika maeneo ya mashinani yalichangia matumizi mapana ya lugha hii. Kwa jumla, matokeo yalionyesha kuwa wingilugha una athari chanya au hasi kwa utekelezaji wa maendeleo kulingana na jinsi lugha husika zinavyotumika katika mawanda mbalimbali. Matokeo ya utafiti huu yatawasilishwa kwa waundaji sera wa Kaunti ya Machakos ili kuwaarifu kihakikifu vigezo sahihi vya uteuzi wa lugha katika mchakato wa kuunda na kuwasilisha sera za maendeleo kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa
maendeleo. Matokeo haya pia yatairutubisha taaluma ya isimujamii.